Utamu wa Lugha
Zuhura Seng’enge
27 August 2026
Nimeujua utamu, kamwe sitaki ukosa,
Na huzidi hio tamu, ulimi unaponesa,
Huwa unaleta hamu, nyoyo kuzitikisa.
Ukikugusa kinywani, hauishi asilani,
Hautoacha tamani, ladha yake mdomoni,
Kwa nafsi ni burudani, huwa ni yenye amani,
Utamu wa lugha.
Utamu wa lugha ni sura yake, uichore kwa maneno,
Utamu wa lugha tabasamu, kung’ara ng’ara kwa meno.
Hujipamba kwa mitindo, na sura za kuvutia,
Wake ni wa pole mwendo, kwa vituo ‘kinyatia,
‘Kihamasisha vitendo, na kuamsha hisia.
Tena huja na mapambo, kwa wale walo mahiri,
Watunzi wa nzuri nyimbo, mashaha wa mashairi,
Wafumbao na mafumbo, mambo yasiwe dhahiri,
Wakivifanya ni vyombo, jamii kuiathiri,
Utamu wa lugha.
Utamu wa lugha uivae, ikukae kama nguo,
Utamu wa lugha mseto; kizamani, kileo.
Kwa wale wapendanao, ndio haswaa burudani,
Wakisemezana yao, pale kwao barazani,
Hutuliza nyoyo zao, kuwaacha furahani,
Kweli hukupa matunzo, hadhi ‘kikunyanyulia,
Indhari na mafunzo, maarifa ‘kujazia,
Lugha ndiyo yako tuzo, huilinda historia,
Utamu wa lugha.
Utamu wa lugha ikuliwaze ukatulia,
Utamu wa lugha ni siri zake, ikikufunulia.
Nimeujua utamu, hakika umenitosha,
Kwa sauti na kalamu, rohoni unanikosha,
Pokea zake salamu, wino nilipodondosha,
Utamu wa lugha, Kiswahili, ukijua kukisuka
Utamu wa lugha kuizungumza kwenye jukwaa, ikasikika.
Utamu wa lugha.
Zuhura Seng’enge, maarufu kama “The African Lioness”, ni mzawa wa Tanzania ambaye ni mwandishi na mbunifu wa zaidi ya miaka kumi anayetumia lugha ya Kiswahili na Kiingereza katika kazi zake. Anafahamika zaidi kwa kazi za ushairi, hasa wa jukwaani. Lakini pia ni mwigizaji wa sauti, mshauri na muelimishaji wa masuala ya kibunifu. Zuhura ameshiriki kazi za kiuandishi na za sanaa, programu, matukio na miradi mbalimbali ndani ya Tanzania na Kimataifa. Na kupitia shughuli zake, anaelimisha, kuburudisha, kuliwaza, kuhamasisha na kuibua mijadala kuhusu jamii, utamaduni, maendeleo, kujitambua, na kuleta mabadiliko chanya. Nje ya shughuli zake binafsi, Zuhura pia ni mwanzilishi mwenza wa kikundi cha ASUSA, ambapo anashiriki katika kusapoti kazi za waandishi, kukuza vipaji, na kuimarisha mazingira ya uandishi bunifu Tanzania.
This poem is published in collaboration with ASUSA
*Image by Kaspars Eglitis on Unsplash

